Rose Ndauka
MWAKA 2012 ndio unakatika. Katika tasnia ya filamu Bongo kuna mengi yalitokea na kuandikwa huku mengine yakiishia chini chini. Kuna mabadiliko makubwa katika tasnia ya filamu kimauzo na ubunifu wa msanii mmoja mmoja, pia kulikuwa na huzuni kutokana na matukio ya hapa na pale yaliyotokea.
SAFARI
Msanii Yvonne Cherryl Monalisa na Steve Kanumba (marehemu sasa) walisafiri kikazi kwenda Uganda kwa ajili ya kufanya usahili wa kushiriki katika filamu ambayo ilishirikisha wasanii nyota kutoka nchi kadhaa zikiwamo Nigeria, Ghana na Afrika Kusini.
Katika safari hiyo pia wasanii kama Rose Ndauka na Lucy Komba walikuwamo, ilikuwa ni kwenda kujaribu bahati yao.
Katika safari hiyo, mwanadada Lucy Komba alipata nafasi ya kuingia mkataba na kampuni ya nje na kurekodi filamu ya Escape To Africa.
FILAMU
Filamu zilizotikisa na kuuzwa sana zilikuwa Tax Driver , Principle Of Women, Nakwenda Kwa Mwanangu, Pastor Myamba The Trial na Ndoa Yangu ambayo ni kati ya filamu zilizoachwa na Kanumba.
Filamu ya Chungu iliyotengenezwa na Dr. Vicensia Shule, iliibuka Filamu Bora kwa mwaka 2012 katika tuzo za Zanzibar International Film Festival (ZIFF).
VIFO
Misiba ilitikisa mwaka huu, mwezi wa Aprili msanii nguli katika tasnia ya filamu Swahiliwood, Steven Kanumba, alifariki dunia baada ya kujigonga katika tendegu la kitanda.
Inadaiwa alisukumwa na msanii mwenzake, Elizabeth Michael Lulu. Msiba huo ulizua hisia za Watanzania na kuandika historia nchini kwa msanii huyo kuzikwa na mamia ya watu.
Kesi ya tukio hilo inaendelea mahakamani huku Lulu akishikiliwa rumande kwani kwa mujibu wa sheria za Tanzania, tuhuma zinazomkabili hazina dhamana.
Vifo viliendelea ambapo msanii mkongwe katika maigizo na filamu Mlopelo naye alifariki. Kana kwamba hiyo haitoshi, wiki hiyo hiyo msanii John Maganga naye alifariki baada ya kuugua.
Huzuni ilizidi kutawala pale msanii nyota wa vichekesho na muziki, Sharo Milionea, alipopata ajali ya gari eneo la Maguzuni Mkoani Tanga iliyosababisha kifo chake.
Sharo naye aliandika historia katika kijiji alichozaliwa cha Lusanga kwani alizikwa na mamia ya watu. Inaelezwa umati ule haukuwahi kutokea kabla si kijijini hapo tu, bali Tanga nzima.
MAHUSIANO
Mahusiano nayo yalishika kasi kwa wasanii huku baadhi yao wakibadilisha dini baada ya kupata mapedejee, baadhi walitangaza uhusiano wao kwa mbwembwe.
Wasanii walioandikwa sana katika hilo walikuwa Jack Wolper aliyetangaza kuolewa na Dallas, lakini hatimaye ndoa hiyo iliota mbawa, Aunty Ezekiel naye aliingia katika mkumbo huo, lakini yeye alifanikisha ndoa umangani alipoona na Sunday.
Rose Ndauka yeye alibadili dini kwa ajili ya kufunga ndoa, hata hivyo bado ndoa hiyo haijafungwa.
MARADHI
Kama walivyo binadamu wengine, wasanii nao maradhi hayakuwaacha. Sajuki ambaye alipata maradhi ya uvimbe tumboni, ndiye aliyeongoza katika hili.
Alitibiwa nchini na ikashindikana, akalazimika kuhitaji matibabu nje ya nchi na kusafirishwa India baada ya Watanzania kumchangia. Alipata matibabu na kurudi akiwa na nafuu kabisa.
Mzee Small naye anasumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi mpaka sasa.
MIKASA
Kuna baadhi ya wasanii hasa wa kike waliandamwa na kashfa, hawa walioongozwa na Aunty Ezekiel na Wema Sepetu waliovuma kwa kupigwa picha za nusu utupu wakiwa jukwaanki. Ingawa waliomba radhi, lakini jamii iliwatafsiri vibaya.
Mikasa haikuishia hapo, kwa mara ya kwanza wanawake katika tasnia ya filamu waliendelea kukumbwa na balaa pale mabinti wawili walipojikuta wakisota lupango hadi sasa.
Nao ni Elizabeth Michael Lulu anayetuhumiwa kuhusika na kifo cha msanii mwenzake, Steven Kanumba na Kajala Masanja anayetuhumiwa kwa kesi ya kutakatisha fedha za Takukuru na kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu.
WALIONG'ARA
Kwa mwaka huu unavyoongelea wasanii walioshika katika tasnia ya filamu kwa upande wa wanaume ni JB, Steven Kanumba, Hisany Muya Tino, msanii chipukizi Slim Mrisho, Baga, Kapturado, Yusuf Mlela, Hemed Suleiman, Richie, Richard Mshanga Mzee Masinde ambaye ndiye Mwigizaji Bora wa Kiume tuzo za ZIFF mwaka 2012, huku wasanii wasiotabirika kama Ray wakiendelea kufanya vizuri.
Kwa upande wa kina dada kama kawaida msanii asipotea katika fani Monalisa alikuwa kinara Jack Wolper aliwafunika wenzake, Jenifer Kyaka Odama Mariam Ismail, Riyama Ali bado nyota yake inaendelea kuwaka, Aunty Ezekiel naye hakuwa nyuma huku Wema Sepetu akifanya vizuri Elizabeth Michael Lulu aliongelewa kwa mwaka huu.
Pia kuna wale wasanii wenye mvuto ambao hata bila ya kufanya kazi nyingine huwa hawaachwi kuwa midomoni mwa watu. Hapa unakutana na mwanadada nyota, Irene Uwoya na Shilole anayejiongezea umaarufu kwa kukata viuno jukwaani.
KING MAJUTO
Msanii mkongwe Amri Athuman King Majuto alishindwa kuficha hisia zake kwa kifo cha meneja wake, Sharo Milionea, aliyepoteza maisha katika ajali ya gari.
Habari za kifo hicho zilimfanya Majuto kuzimia, katika mahojiano baadaye Majuto alisema licha ya tofauti yao kubwa ya umri, lakini Sharo ndiye aliyemsababisha aijua thamani yake kwa kumwingiza katika mikataba minono ya kazi.
FARAJA
Serikali ya Tanzania ilitangaza kuitambua tasnia ya filamu kuwa ni sekta rasmi na kutangaza kuwa kuanzia mwakani Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itaingia rasmi kwa ajili ya kuweka alama ya utambulisho katika harakati ya kupambana na maharamia wa kazi za wasanii kwa kushirikiana taasisi husika.
No comments:
Post a Comment