Monday, December 24, 2012

PICHA 5 NA MAELEZO YA KILICHOSABABISHA SAJUKI KUANGUKA JUKWAANI


KWA mara nyingine tena, hali ya staa wa filamu za Kibongo, Juma Kilowoko ‘Sajuki’ (pichani) imewazidishia hofu Watanzania baada ya kuanguka jukwaani akiwa jijini Arusha, Amani linakujuza.
Sajuki baada ya kuanguka chini.
Tukio hilo lilitokea katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa hivi karibuni kulipokuwa na tamasha lililowahusisha wasanii wa sinema ambapo Sajuki alitakiwa kupanda jukwaani ili kusalimia kadamnasi.
Cha ajabu, baada ya kukabidhiwa kipaza sauti, Sajuki hakuweza kuongea, badala yake alipaza sauti na kupiga kelele kisha kuanguka chini, hali iliyozua hofu uwanjani hapo.
Baada ya tukio hilo, Sajuki ambaye ni mgonjwa kwa muda mrefu sasa, alichukuliwa na wasanii wenzake na kuwekwa pembeni kwa ajili ya huduma ya kwanza.
Miongoni mwa maneno yaliyomtoka kinywani kwa wakati huo ni haya: “Sijisikii vizuri, hali yangu ni mbaya.”
Baadhi ya watu waliohojiwa na Amani, walisema msanii huyo anapaswa kufanyiwa maombi maalum ili aweze kupata nguvu za kuendelea kufanya shughuli zake.
Wadau wakijaribu kumnyanyua Sajuki baada ya kudondoka jukwaani.
“Mungu amuongoze lakini anahitaji maombi kwa kweli. Si suala la daktari peke yake,” alisema Mary Shimo, mkazi wa Kijenge jijini hapa.
Hata hivyo, baadhi ya madaktari walioongea na mwandishi wetu walisema wanashangazwa na tabia ya  msanii huyo kuzunguka mikoani na wasanii wenzake huku afya yake  ikiwa mgogoro.
“Sajuki bado hajapona, muda mwingi anatakiwa apumzike kuliko kusafiri kama anavyofanya,” alisema mmoja wa madaktari hao.
Hivi karibuni, Sajuki na baadhi ya wasanii wa filamu walifanya ziara mjini Iringa na msanii huyo alianguka jukwaani kama ilivyomtokea jijini hapa.
Habari zilizopatikana wakati tunakwenda mitamboni zinasema, zinatakiwa shilingi milioni 18 ili msanii huyo arudi India kwa ajili ya kuendelea na matibabu.
Mei mwaka huu, Sajuki alikwenda nchini India kwa lengo la kutibiwa, lakini ikasemekana alirudishwa ili atimize baadhi ya mambo kabla ya kwenda kufanyiwa matibabu kamili.
Simon Mwakifwamba (kushoto) na wadau wakimpa kampani Sajuki kutoka jukwaani.

No comments:

Post a Comment