BADO tupo mwanzoni mwa mwaka lakini tukio la maiti ya kichanga kugeuka jogoo ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam linaweza kuongoza mengine yote ya ajabu yanayoweza kujiri ndani ya 2013.
Asubuhi ya Jumatano iliyopita, ilikuwa kizaazaa pale jokofu lililotumika kuhifadhi maiti ya kichanga cha mtoto, kukutwa kuna jogoo.
Mshangao zaidi ni kwamba ndani ya lile jokofu, pembeni ya yule jogoo, kulikuwa na hirizi pamoja na tunguri.
Habari kutoka vyanzo vyetu, zimewekwa wazi kuwa Jumanne iliyopita, saa 7 mchana, polisi walipigiwa simu, wakataarifiwa kuhusu maiti ya mtoto iliyokuwa imetelekezwa eneo la Kigogo, Mbuyuni, Dar es Salaam.
Vyanzo vyetu vimebainisha kuwa polisi baada ya kupata taarifa hizo walifika eneo la tukio na kukuta maiti hiyo ya kichanga ikiwa imefunikwa kwa kuzungushiwa sanda.
Kwa mujibu wa Moses Madilu, mkazi wa Kigogo, aliyedai kushuhudia tukio hilo, polisi walipofika eneo la tukio waliikagua maiti hiyo na kubaini kwamba ni ya kike.
Chanzo chetu kikaeleza kuwa baadhi ya mashuhuda, hususan wanawake, walitokwa na machozi kwa masikitiko kwamba itakuwa mtu alijifungua halafu akakinyonga kichanga hicho kabla ya kukitelekeza eneo hilo.
“Baada ya kujiridhisha kwa kazi yao, polisi waliichukua maiti hiyo ya kichanga, wakaipakia kwenye ‘difenda’, wakaipeleka Hospitali ya Mwananyamala,” kilieleza chanzo chetu.
HOSPITALI YA MWANANYAMALA
Ndani ya hospitali hiyo, mwandishi wetu alielezwa kuwa polisi walipofika, walishusha maiti hiyo na kumkabidhi mganga wa zamu aliyejulikana kwa jina moja la Dk. Liwa.
“Dk. Liwa aliwaambia wale polisi wapeleke maiti hiyo mochwari.
“Polisi walifanya hivyo lakini kule mochwari walimkuta msimamizi mkuu, Omar Buyoya aliyekataa kuipokea kwa vile daktari hakuthibitisha kama kile kichanga kilikufa au kilikuwa hai.
“Polisi na Buyoya walivutana kwa muda mrefu, alitokea mhudumu mwingine wa mochwari aliyekuwa akijuana na polisi mmoja aliyebeba ile maiti, alikubali kuupokea mwili huo na kuingiza ndani kwenye jokofu la kuhifadhia maiti.”
Muuguzi huyo aliendelea kusema kuwa siku iliyofuata, Dk. Liwa alifika mochwari na alipofungua jokofu na kufunua sanda, badala ya kukuta maiti ya kichanga, alikuta jogoo, tunguri na hirizi.
“Dk.Liwa alipatwa na mshangao mkubwa huku jasho likimtoka kutokana na uoga, aliwaita wafanyakazi ambao walijazana hapo mochwari kushuhudia.
“Baadhi ya wafanyakazi walipigwa na butwaa huku wengine wakicheka hadi kudondoka chini na wakawa wanajiuliza kama kweli polisi wanaweza kupeleka jogoo hospitali au ni mambo ya kishirikina,” alisema muuguzi huyo.
Dk. Liwa na wafanyakazi wenzake waliondoka mochwari na kuacha hilo jogoo katika chumba cha maiti huku wakishindwa la kufanya.
KAULI YA MGANGA MKUU.....
Uwazi ilimtafuta Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk. Sophinias Ngonyani ambaye alikiri kuonekana kwa jogoo badala ya maiti ya kichanga.
“Polisi walituletea kifurushi wakiamini kuwa ni maiti ya kitoto kichanga ambapo tulikipokea lakini ilipotazamwa na daktari, tulikuta jogoo, hirizi na tunguri, tuliamua kumchoma moto kwa sababu kile ni chumba cha kuhifadhi maiti siyo cha kuhifadhia mizoga ya kuku, ng’ombe au mbwa,” alisema Dk. Ngonyani.
KAULI YA POLISI ...
Naye Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela alipoulizwa juu ya sakata hilo alisema kwamba wao kama jeshi la polisi walipigiwa simu na raia mwema kuwa kuna maiti ya kichanga ambapo askari waliondoka hadi eneo la tukio na kuichukua mpaka Hospitali ya Mwananyamala.
“Polisi waliichukua hadi Hospitali ya Mwananyamala kwa wataalamu na baada ya kuikabidhi waliondoka na kuendelea na shughuli nyingine, nami nashangaa kusikia kwamba madaktari walikuta jogoo,” alisema Kenyela.
MASWALI MATANO
Je, ni kweli polisi waliikagua maiti na kugundua ni kichanga cha kike?
Kama ndiyo, ilikuwaje kikageuka jogoo?
Kwa nini daktari hakuipima ile maiti, badala yake akaelekeza ipelekwe mochwari?
Je, au polisi walibeba mzoga wa jogoo, wakampakia kwenye difenda wakidhani ni maiti ya kichanga?
Mkweli nani, polisi wanaodai kupeleka maiti ya kichanga, au hospitali wanaosema walipelekewa mzoga wa kuku, tunguri na hirizi?
SOURCE: GPL
No comments:
Post a Comment