Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, amemtaka Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, kuwaeleza wananchi hatua alizochukua hadi sasa dhidi ya ubinafsishwaji wa Kiwanda cha Nguo cha Urafiki. Mnyika aliyasema hayo katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Saalm jana baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara, Mahmoud Mgimwa, kukaririwa na moja ya vyombo cha habari, akidai kuwa kamati ndogo iliyoundwa kuchunguza ufisadi wa miaka mingi wa kiwanda hicho unasubiri idhini ya Spika wa Bunge ili kuanza kazi.
“Nikiwa Mbunge wa jimbo kilipo kiwanda cha Urafiki, nasisitiza umuhimu wa Spika kutoa kauli kwa umma kuhusu hatua alizochukua ikizingatiwa kwamba hata kabla ya kamati ndogo ya uchunguzi kuundwa nilishawasilisha kwa Spika wa Bunge maelezo binafsi kuhusu ufisadi huo na mpaka sasa hajatoa idhini yashughulikiwe,” alisema.
Aidha, Mnyika alisema majibu ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdalah Kigoda ya kufuatilia suala hilo wizarani, hayajitoshelezi kutokana na kuahidi kulifutilia suala hilo zaidi ya nusu mwaka sasa.
“Wananchi na wafanyakazi wa kiwanda hicho wanahitaji kufahamu hatua zilizochukuliwa mpaka sasa ili kukinusuru kiwanda hicho,” alisema Mnyika.
Pia ameitaka serikali kuweka hadharani ripoti ya matumizi ya mkopo wa dola milioni 27 (takribani Sh. Bilioni 40), ambazo zilitumika kununua mitambo chakavu kutokana na mianya ya ufisadi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment