HATUA ya mwanazuoni wa siku nyingi nchini, Profesa Issa Shivji kupinga
hukumu ya Mahakama ya Rufani Tanzania iliyomrejeshea ubunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema imemtia matatani na baadhi ya watu wanasema gwiji
huyo wa sheria “huenda amenukuliwa vibaya au hajasoma hukumu husika.”
Jana
Wakili wa Lema, Tundu Lissu, alimkosoa Profesa Shivji pamoja na Rais wa
Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, Francis Stolla akisema wanasheria
hao wamepotoka katika matamshi yao ya kupinga hukumu ya Mahakama ya
Rufani.
Matamshi ya Shivji pia yaliiteka mijadala katika mitandao
ya kijamii ya Jamii Forums, Mabadiliko na Facebook ambako wachangiaji
walikuwa wakivutana huku baadhi yao wakisema wazi kwamba msomi huyo
amekosea huku wengine wakimtetea kwamba yuko sahihi.
Akizungumza
na gazeti hili jana kutoka Songea mkoani Ruvuma, Lissu alipinga vikali
hoja zilizotolewa na Profesa Shivji pamoja na Stolla, akisema kuwa
hazina mashiko na zinaweza kutolewa tu na mtu ambaye hakufuatilia
mwenendo wa kesi hiyo.
Juzi Profesa Shivji na Stolla walinukuliwa
wakiikosoa hukumu ya Mahakama ya Rufani, iliyomrejesha bungeni Lema
wakisema hukumu hiyo iliyotolewa na majaji watatu Salum Massati, Bernard
Luanda na kiongozi wao Nathalia Kimaro, inapingana na sheria.
Lissu
katika maelezo yake alisema uamuzi wa mahakama katika kesi ya Lema
umejenga upya msingi bora wa matumizi ya vyombo vya uamuzi, kwani kesi
nyingi za kupinga matokeo ya ubunge, zimekuwa zikifunguliwa na watu
ambao wamekuwa wakitumwa na vigogo wa kisiasa na watu wenye fedha.
Akizungumza
na Mwananchi, Lissu alisema hoja hizo hazina mashiko na kuwa ile
iliyotolewa na Profesa Shivji inatokana na msomi huyo kuzungumza
kitaalamu bila kuangalia mazingira halisi ya siasa za Kitanzania.
Lissu
alisema mahakama ya rufani haikupiga marufuku wapiga kura kufungua kesi
za kupinga ila iliwataka tu kufanya hivyo pale haki zao zinapokiukwa.
“Kwanza
siyo kweli kwamba mahakama imepiga marufuku wapiga kura kufungua kesi,
ilisema watafanya hivyo pale ambapo haki zao zimevunjwa, haki zenyewe ni
kupiga kura, kura zao kutohesabiwa ama suala jingine litakalomnyima
kupiga kura, hizo ndiyo haki za mpiga kura,” alisema na kuongeza:
“Sasa
mwalimu wangu, Profesa Shivji yeye anatazama tu kwa jicho la kitaalamu
na kusema haki za binadamu zimekiukwa, kwa muda wanasiasa, matajiri na
CCM wamekuwa wakiwatumia wananchi kuwapinga wabunge wa upinzani.”
Uchambuzi wa Lissu
Alitoa
mfano akisema katika uchaguzi wa 1995, Dk Willibrod Slaa alishinda
ubunge na watu wanaojiita wananchi walifungua kesi kupinga ushindi huo,
mwaka 2000 wakampinga tena na hata 2005.
Alisema 1995 Makongoro
Nyerere aliposhinda ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini kupitia NCCR-
Mageuzi, watu wanaojiita wananchi walifungua kesi ambayo matokeo yake
yalikuwa mbunge huyo kupoteza kiti chake.
Lissu alisema 2005
aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Marehemu Chacha Wangwe alifunguliwa kesi na
watu waliojiita wananchi ambao mwisho wake walishindwa.
No comments:
Post a Comment