Mbunge wa
Jimbo la Kawe katika Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam, Halima
Mdee amewataka wakazi wa Chasimba, Chatembo na Chachui kutoa ushirikiano
katika zoezi la uthamini wa maeneo yao yenye mgogoro wa muda mrefu na
kiwanda cha saruji cha Wazo Hill. Mdee
aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara na wananchi hao ambao
ulifanyikia kwenye viwanja vya Serikali ya Mtaa ya Basihaya iliyopo
Chasimba na kuhudhuriwa na madiwani, John Morro wa kata ya Wazo na
Sharif Majisafi wa kata ya Bunju.
Mdee
akiwahutubia wananchi hao alisema kuwa licha ya kuwepo na hukumu ya
Mahakama ya Rufaa iliyowapa ushindi kiwanda cha saruji cha Wazo Hill
dhidi ya wananchi hao, lakini hakuna mwananchi atakayeondoka katika
maeneo hayo.
"Kwa kuwa tayari mlishakubaliana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka wakati alipokuja kuhusiana na
kuwekwa mipaka na kufanyika kwa zoezi la uthamini, acha lifanyike ili
msionekane ni vikwazo lakini huku kwenye vichwa vyenu mkiwa mnaelewa
kuwa hakuna mwananchi atakayetoka hapa maana linafanyika na nyinyi mkiwa
humu," alisema Mdee.
Alisema kuwa tathmini ni kutimiza matakwa kisheria kutokana na nchi
kuendeshwa kwa sheria, hivyo hakuna sababu ya kulikataa zoezi hilo
ambalo linaonyesha serikali kama ina nia nzuri ya kutaka kumaliza
mgogoro huo wa muda mrefu kati ya kiwanda cha Wazo na wananchi wa maeneo
hayo.
"Serikali inaonekana kama inataka kumaliza mgogoro kati yenu na kiwanda
cha Wazo, hivyo tuwape ushirikiano katika zoezi hilo, twende nao lakini
tukiona njia tunayokwenda nao si nzuri kila mmoja 'asepe' na njia yake,"
alisema.
Aliongeza kuwa maeneo hayo kufanyiwa tathimini inaweza kuwa neema kwa
wakazi hao kuweza kupata huduma nyingi ikiwemo umeme na maji kwa njia za
haki badala ya njia za panya kama ilivyo sasa.
Mdee alisema kuwa nyaraka zilizopo sasa zinaonyesha kuwa maeneo hayo
yapo katika eneo la kiwanda, hivyo ili yatengane na eneo la kiwanda ni
lazima mipaka iwekwe na tathimini ifanyike.
"Sisi viongozi wenu tupo na nyinyi kwa asilimia mia moja na msimamo wetu
ni nyinyi kubaki katika maeneo haya, kama serikali ilifanya uzembe
kummilikisha mwekezaji eneo kubwa kwa njia inazojua yenyewe imlipe fidia
aondoke nyinyi mbaki na si vinginevyo," alisema.
No comments:
Post a Comment