Wednesday, January 23, 2013

HIZI NDIO MBINU ZA KUANZISHA BIASHARA ENDELEVU





Na Charles Msuluzya Nazi
17. Mazao ya chakula
Biashara ya kununua na kuuza mazao ya chakula ni biashara nzuri ambayo ina faida kubwa na pia soko lake ni la uhakika kwa sababu kila mtu anahitaji chakula. Bei za mazao huwa zinabadilika mara kwa mara kufuatana na msimu. Kwa mfano; wakati wa mavuno mazao huwa na bei ndogo na kupatikana kwa wingi ubunifu ni kuhamisha kutoka huko kwenye wingi na kuyauza kwenye uhaba kwa faida kubwa. Au unaweza kununua kwa wingi na kuhifadhi hadi msimu wa uhaba nawe ukauza kwa faida kubwa. Biashara hii inahitaji uwe na mtaji pia na maghala ya kutunzia mazao hayo. Unapaswa kujifunza mbinu za kuhifadhi mazao kama vile kuweka dawa za kuua wadudu ili mazao yasiharibike. Unaweza ukaamua kuwa mkulima wa mazao, kuyalima na kuyauza au kununua mazao na kuyauza. Ni muhimu kufanya utafiti wa soko la mazao yako kabla ya kufanya biashara hii ili usije ukashindwa kuyauza.

18. Huduma za kitaalamu.
Biashara ya kutoa huduma za kitaalamu ni nzuri sana na ina mapato mazuri, inaweza kuleta utajiri na maisha bora. Ili ufanye biashara hii unapaswa kwanza kusomea taaluma husika kwa kiwango kinachohitajika na wahitaji au masoko. Taaluma ambazo zina malipo mazuri ni ufundi, ualimu, uanasheria, udaktari ufamasia, uhasibu na ufundi wa vifaa vya elektroniki. Unaweza kuanza kwa kuajiriwa kwenye ofisi inayotoa huduma ya fani yako ili upate uzoefu na siri ya biashara hiyo. Kisha tafuta kuanza taratibu kufanya kazi zako binafsi. Ukiona biashara yako inaenda vizuri acha kazi na uende kufanya biashara yako kwa juhudi na maarifa yako yote na utafanikiwa.

19. Magari ya usafirishaji.
Biashara ya usafirishaji ni biashara pana sana ambayo inajumuisha magari ya abiria na magari ya mizigo. Ni biashara yenye faida sana, inayohitaji mtaji mkubwa na usimamizi wa hali ya juu ili kudhibiti wizi wa mapato. Kwa kuwa biashara hii ni pana kila aina ya biashara tutaizungumzia hapa nchini.

(i) Kusafirisha abiria
Biashara hii ni nzuri na inayo mapato mazuri ya uhakika. Ili uweze kufanikiwa katika biashara hii unatakiwa ununue gari ambalo ni zima. Usimamie kwa karibu na kudhibiti mapato ili yasiibiwe. Gari linatakiwa lifanyiwe ukarabati mara kwa mara ili liwe katika hali nzuri ya kufanya kazi. Uweke akiba nusu ya mapato ili kukabiliana na dharura ya matengenezo makubwa. Niliwahi kuzungumza na aliyekuwa mmiliki mmoja wa magari ya kusafirishia abiria kuhusu suala hili ambapo alisimulia mkasa uliomkuta. Yeye alikuwa analetewa mapato yake katika kumbi za starehe na kutumia hizo fedha, kunywea pombe. Alikuwa haweki akiba. Siku moja gari liliharibika na lilihitaji matengenezo ya Tshs 900,000/=. Mmliki huyo wa magari ya kusafirishia abiria alikuwa hana fedha hivyo aliamua kuuza gari. Matatizo ya aina hii ya biashara ni kuwapo watu wengi wanaotegemea kuchota mapato hayo nao ni dereva, kondakta, mawakala na kadhalika. Pia kuna udanganyifu mwingi unaofanywa na dereva na kondakta kwa kusingizia kuwa gari limeharibika au limekamatwa na askari wa usalama barabarani wakati siyo kweli ili mapato wayaibe. Pia kuna wizi wa mafuta na vipuri. Ili kukabiliana na matatizo haya unaweza kumwekea kiwango maalum cha mapato anayopaswa kuwasilisha na dereva na kondakta. Kwa mfano, kwa gari la uwezo wa kubeba abiria 18 kiasi cha mapato ni Tshs 25,000/= kwa siku na gari la abiria 26 mapato ni Tshs 40,000/= kwa siku. Pia unapaswa kufuatilia nyendo za wafanyakazi hao. Unaweza kuingia mikataba na makampuni ya kusafirisha wafanyakazi au wanafunzi ili upate mapato ya uhakika pia.

(ii) Magari ya kukodi
Biashara ya taxi ni nzuri na ina faida kubwa. Tatizo lake ni gumu kudhibiti kwani soko la abiria halina uhakika kama magari ya abiria ni rahisi dereva kukuambia kwamba hajapata abiria siku nzima. Pia kuna wizi wa mafuta na udanganyifu kwa kisingizio cha kuharibika gari. Katika biashara hii unatakiwa ununue gari zima, ulifanyie ukarabati mara kwa mara ili liwe katika hali nzuri ya kufanya kazi.Umfuatilie dereva wako katika nyendo zake ili uwe karibu nae kwa msaada atakaotaka na urejeshaji mzuri wa mapato. Unaweza kudhibiti mapato kwa kumwekea dereva wa taxi kiwango cha mapato cha kuwakilisha kwa siku ambazo ni Tshs 10,000/= Unaweza kuingia mkataba wa kukodisha kwenye makampuni kusafirishia watalii au wageni na kupata mapato ya uhakika.

(iii) Magari makubwa ya abiria
Biashara hii ni nzuri. Inahitaji mtaji mkubwa kwani gari moja, linaweza kununuliwa hadi kwa Tshs 100,000,000/= Inahitaji uthibiti wa mapato kwa hali ya juu kwani kuna watu wengi ambao wanategemea kuchota mapato ya gari kama vile dereva, kondakta, mawakala, wahudumu wa magereji na kadhalika. Kuna udanganyifu mwingi unaofanywa na wafanyakazi li wakuibie, kama vile kusafirisha abiria wa njiani na mizigo. Bila kuonyesha ankara na wafanyakazi kuchukua fedha za nauli bila kuziwasilisha. Pia kuna wizi wa mafuta, kusingizia gari kuharibika wakati ni zima au kusingizia kukosa abiria ili wachukue fedha za nauli. Ili kukabiliana na matatizo hayo unapaswa: kununua gari zima na kulifanyia ukarabati mara kwa mara ili gari liwe katika hali nzuri ya kufanya kazi. Simamia gari lako kuhakikisha linajaza abiria kabla ya safari. Unaweza kuweka wakaguzi na kufanya ukaguzi wa kushitukiza njiani ili kubaini udanganyifu wa kupakia abiria wa njiani na mzigo bila kuwakatia tiketi. Weka akiba nusu ya mapato kukabiliana na gharama za matengenezo makubwa au dharura. Ajiri wafanyakazi waadilifu na pia uwalipe vizuri na uwape motisha. Ii kujipatia mapato ya uhakika, kama una magari mengi unaweza kuingia mkataba na watu binafsi au makampuni kusafirisha wafanyakazi au wanafunzi.

(iv) Magari ya mizigo
Biashara hii ni nzuri. Ina faida kubwa pia. Wingi wa mapato unategemea na ukubwa wa gari. Ili ufanikiwe katika biashara hii, unapaswa kununua gari zima kulifanyia ukarabati kila mara ili kuliweka katika hali nzuri ya kufanya kazi. Pia unatakiwa kutafuta wateja wa kukodisha gari lako kwa kungia mkataba na wafanyabishara ili kuwasafirishia mizigoyao. Unaweza kuliegesha gari lako sehemu ambayo kuna wateja wanaohitaji kusafirisha mizigo, kama vile sokoni, kwenye maduka ya jumla au viwandani. Matatizo ya biashara hii ni kuwapo kwa watu wengi wanaotegemea mapato ya gari lako ambao ni dereva, utingo, mawakala na kadhalika. Pia kuna udanganyifu unaofanywa na wafanyakazi kama vile, kubeba mizigo bila kuwasilisha fedha, wizi wa mafuta, kusingizia gari kuharibika au kukamatwa askari wa usalama wa barabara wakati sio kweli ili wakuibie fedha za usafirishaji wa mizigo. Ili kukabiliana na tatizo hili ajiri wafanyakazi waaminifu, uwape motisha na kuwalipa mshahara mzuri. Unapaswa pia kufuatilia nyendo za wafanyakazi wako.Tafuta pia wafanyabishara wakubwa au mashirika kusafirisha mizigo yao ili upate mapato ya uhakika.
CHARLES MSULUZYA NAZI
Mwandishi wa makala hii ni mshauri wa biashara na mtunzi wa kitabu cha Mbinu za biashara na maarifa ya kupata pesa na utajiri. Kwa mawasiliano piga simu namba 0755394701 barua pepe cnazi2002@yahoo.com http://www.squidoo.com/mshauricharles

No comments:

Post a Comment