Saturday, January 26, 2013
HUYU NDO BIBI KUTOKA MTWARA MWENYE UWEZO WA KUBADILI GESI KUA MAJI
Bibi Somoye Issa (90).
Kwa mujibu wa wanakijiji hao, Mtu huyo ambaye ana asili ya kijiji hicho
waliyemtambua kwa jina la Seleman Babu aliwasili kijijini hapo jana saa
10 jioni akiwa na gari ndogo aina ya Mark II na kwenda nyumbani kwa
shangazi yake.
Habari zinadai kuwa saa 2 usiku Babu, alikwenda nyumbani kwa Bibi Mtiti
akiwa na gari pamoja na shangazi yake aliyetajwa kwa jina la Fatuma
Saidi Tom.
Mkazi wa kijiji hicho, Juma Ayoub alisema: “Unajua yule bibi tunamlinda,
sasa ilipoonekana ile gari usiku pale, watu wakaanza kujiuliza
linafanya nini? Wakaanza kusogea, kadiri muda ulivyokwenda ndivyo watu
walivyozidi kuongezeka.”
Asha Hamisi, mtoto wa pili wa Bibi Mtiti, akihadithia juu ya tukio hilo
alisema yapata saa 2 usiku wakiwa wanakula chakula alipokea wageni
wawili ambao baada ya kumaliza kula waliomba kuongea na Mkuu huyo wa
Kaya. “Alikuja kijana na mama wakaniomba kuongea na bibi… Alimuliza
bibi kama ana uwezo wa kwenda Mtwara, bibi akajibu hawezi… Wakaniuliza
mimi kama naweza kwenda badala yake nikawaambia siwezi… Akasema
ametumwa na Rais Jakaya Kikwete na Hawa Ghasia wamjie bibi wakazungumze
naye mambo ya gesi… Alisema kama bibi yupo tayari Jumanne ijayo
watamfuata kwa gari, mimi nikasema sitaki, nilipochungulia nje nikaona
watu wengi wamezunguka.”
Manzi Mohamedi Faki mtoto wa tano wa Bibi Mtiti anasimulia: “Kwa kuwa
tunamfahamu tulimwambia aondoke mpango aliojia haufai, akawa anabisha,
tukaendelea kumsihi, wakati huo watu wanazidi kuongezeka, alipotoka
akakosea njia, alipopita hakukuwa na njia, watu walimfuata wakaanza
kumrushia mawe, aliacha gari akakimbia, ndipo wananchi walipoliteketeza
gari kwa moto.”
Fatuma Tom ambaye ni shangazi wa Babu amethibitisha kumpokea mwanae huyo
na kumsindikiza kwa Bibi Mtiti na ambako alimuomba mkuu huyo wa kaya
akubali kuondoka nae kwenda Dar es Salaam kwa maelezo kuwa ametumwa na
viongozi wake wa juu: “Ni mwanangu mtoto wa kaka yangu, alikuja
akaniomba nimepeleke kwa bibi akamsalimie tuliondoka saa 2 usiku…watu
walituzingira na hali ilipokuwa mbaya niliondoka na kumwacha mwanangu
pale, nae alikimbia na ndipo walipochoma moto gari…. Huyu mwanangu
anaishi Dar es Salaam, anafanya kazi usalama wa Taifa…nadhani alirudi
jana hiyohiyo Mtwara.”
Mwenyekiti wa kijiji cha Msimbati, Salum Tostao alithibitisha kutokea
kwa tukio hilo na kuongeza kuwa ofisi yake haikupokea mgeni yeyote
kutoka serikalini kwa siku hiyo: “Ni kweli gari imechomwa lenye namba za
usajili T 609 BXG mali ya Mussa Babu…taarifa hii ni kwa mujibu wa
nyaraka tulizookota kutoka ndani ya gari hilo.”
Selemani Babu alikanusha madai ya yeye kwenda kijijini hapo jana na
alisema: “Hapana, hapana labda umekosea…na… na… na… umekosea…
sijakwenda Msimbati jana… kwanini asiwe Mussa, umekosea sio mimi
kwaheri.”
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuki alisema hana taarifa
zozote kuhusiana na tukio hilo kwa kuwa mhusika hajaenda polisi
kulalamika.
Pichani juu ni Aisha Hamisi ni mtoto wa pili wa Bibi Mtiti
Wananchi wakitizama mabaki ya gari lililochomwa moto
——————————————–
Baada ya majibizano ya hapa na pale kuendelea kwa muda mrefu baina ya
Serikali, Wanaharakati na Wananchi wa Mikoa ya Kusini sasa inaonekana
mgogoro huo kukua zaidi siku hadi siku. Ililipotiwa hapo kabla kuhusu
Naibu Waziri wa Nishati kwenda usiku huko Msimbati na kufukuzwa,
ingawaje Serikali kwa upande wake ilikanusha habari hiyo na kudai ni
maneno ya kizushi na udanganyifu wa watu kujitafutia umaarufu.
Katika kile kinachoonekana kuwa ni hatari, asubuhi ya leo tumepata
taarifa kwamba gari lililoenda kwa ajili ya kumbeba Bibi kwenda naye
kusikojulikana limechomwa moto. Taarifa zinasema, watu kadhaa akiwemo
kijana mmoja mwenye asili ya ukaazi wa kijiji hicho walikamatwa jana
usiku na wanakijiji cha Msimbati wakidai wameagizwa kuja kumchukua Bibi
huyo ili wakafanye maongezi na Wakubwa ambao pia hawakuweza kuwekwa
bayana ni Wakubwa gani hao. Kinachoelezwa ni kwamba, baada ya mtafaruku
huo, watu hao walichoropoka na kukimbia kitu kilichowapa hasira wananchi
na kuamua kuchoma gali hilo ambalo walikuja nalo.
Wananchi hao wamesema wako tayari kumlinda Bibi huyo usiku na mchana kwa
kuhofia kurubuniwa na Serikali ili abadili msimamo wake.
Ni hatari, kwa sababu mbali na propaganda za viongozi wetu wa Kitaifa
kwamba suala la gesi ni la Wanamtwara Mjini tu; Kwamba wenyewe wa
Msimbati na Mtwara Vijijini kwa ujumla wako tayari gesi hiyo kupelekwa
Dar es salaam, si kweli. Leo hii, wale wanaodaiwa kuwa tayari kuruhusu
gesi hiyo wameteketeza gari, je wale wasio tayari kwa hilo kesho
watafanya nini?
Serikali isidharau wananchi na wale wenye matakwa mema na nchi hii, kwani
mbali
na mamlaka ambayo serikali imepewa katika kusimamia rasilimali za nchi,
bado uhalali wa wamiliki asilia wa rasilimali hizo ambao ni wananchi
hauwezi kuporwa. Wananchi wanaozungukwa rasilimali husika ndio
wamiliki halali wa rasilimali hizo kabla ya Serikali na jamii zingine za
nchi. Hivyo wanufaika wa kwanza wa rasilimali husika ni lazima wawe ni
wale wenye uhalali wa Ki-asili na si vinginevyo.
Tuache dharau!
Leo gari limechomwa, kama hii hali itaendelea kuwa hivi, tusishangae
kuambiwa kuna mtu pia kachomwa au kapoteza maisha kwa sababu hizi hizi
zinazofanyiwa masihara na viongozi wetu.
Tuweni wazalendo, tutetee maendeleo ya nchi na watu wake kwa vitendo, tuache porojo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment