SUALA la Joshua Mulundi anayetuhumiwa kumteka Dk Steven Ulimboka, katika
Misitu ya Pande, limechukua sura mpya baada ya ubalozi wa Kenya nchini
kuamua kumchunguza, ili kubaini kama kweli ni raia wake au la.
Balozi wa Kenya nchini, Mtindo Mutiso aliliambia gazeti hili juzi kuwa
amesikia taarifa za Mulundi akidai kuwa ni raia wa Kenya, lakini kama
nchi, itahitaji kujiridhisha kabla haijajiingiza kumsaidia kwa lolote.
Mtuhumiwa huyo ambaye kwa sasa haijulikani yuko mahabusu gani baada ya
kuhamishwa kutoka Gereza la Keko jijini Dar es Salaam kutokana na
ufuatiliaji wa vyombo vya habari, amenukuliwa mara kadhaa na baadhi ya
magezeti (siyo Mwananchi) kwamba hatendewi haki.
Pamoja na madai mengine, Mulundi amekuwa akitaka Ulimboka apelekwe
mahabusu ili amtambue kama kweli alihusika kumteka, ili haki dhidi yake
itendeke haraka.
Dk Ulimboka alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba muda
kuzungumzia ukweli kuhusu tukio hilo bado na kwamba hajawahi kuitwa, ili
akutanishwe na mtuhumiwa huyo.
Hata hivyo, uongozi wa Magereza nchini ulisema kwamba hauwezi kumsaidia
mtuhumiwa huyo kwa lolote, badala yake ulimtaka aandike barua ya
malalamiko na kumkabidhi mpelelezi wa kesi yake, ili ayafikishe
mahakamani kwa hatua zaidi.
Juzi Balozi Mutiso alisema kwamba kutokana na suala hilo kuendelea kuwa
na utata hasa kuhusu uraia wa mtuhumiwa huyo, aliamua kutuma ujumbe
kwenda Gereza la Ukonga ambako alielezwa kwamba mtuhumiwa huyo
anapatikana, lakini hakufanikiwa kumwona.
“Mimi nilituma kijana wangu leo pale gereza la Ukonga, lakini alipofika
huko akaelezwa hayupo, eti afuatilie vizuri chanzo chake cha taarifa
hizo mahali alipopelekwa. Nikaamua kukupigia simu (gazeti) ili
tusaidiane kujua mahali alipo,” alisema Mutiso.
Mutiso alisema kutokana na hatua hiyo ameamua kufuatilia ili kujua madai
ya mtuhumiwa huyo kuwa raia wa Kenya kabla hajajihusisha zaidi na suala
hilo.
“Taratibu za kibalozi inapotokea jambo kama hilo, ni lazima awepo mtu au
ndugu atakayemtambua kuwa Mkenya, au kupata vyeti vyake vya uraia.
Lakini hatujapatiwa vyeti hivyo. Kwa hivyo tunataka kuthibitisha kwanza
kama ni Mkenya halafu tuhusike zaidi katika suala hulo,” alisema Mutiso.
Mutiso alisema leo atafanya uamuzi wa kufika mwenyewe katika Ofisi za
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ama kuandika barua ya
kutaka uthibitisho wa uraia wa Mulundi.
“Jumatatu (leo) ndiyo nitawasiliana na wizara ili nifahamu kijana huyo yupo katika gereza gani,” alisema Mutiso.
No comments:
Post a Comment