Kocha
Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameondoka leo mchana (Januari 18 mwaka
huu) kwa ndege ya South African Airways kwenda Afrika Kusini
kuzifuatilia timu za Ivory Coast na Morocco zinazoshiriki Fainali za 29
za Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazoanza kesho (Januari 19 mwaka huu)
nchini humo.
Ivory
Coast na Morocco ziko kundi moja na Tanzania (Taifa Stars) katika
kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia
zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, na inayoshika nafasi
ya pili katika kundi hilo ambalo pia lina timu ya Gambia itacheza na
Morocco, Machi 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
RWIZA, LIUNDA KUSIMAMIA MECHI ZA CAF
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limewateua Watanzania Leslie Liunda na
Alfred Rwiza kuwa makamishna wa mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika
zinazoanza mwezi ujao.
Rwiza
ameteuliwa kuwa kamishna wa mechi kati ya APR ya Rwanda na Vital’O ya
Burundi itakayochezwa nchini Rwanda kati ya Februari 15 na 17 mwaka huu.
Naye
Liunda atakuwa kamishna wa mechi ya marudiano kati ya Tusker ya Kenya
na St. Michel United ya Seychelles itakayochezwa Kenya kati ya Machi 1
na 3 mwaka huu. Mechi zote ni za raundi ya awali.
WATANZANIA KUZICHEZESHA URA, COTTON SPORT
Waamuzi
wanne wa Tanzania wameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) kuchezesha mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa kati ya URA ya
Uganda na Cotton Sport ya Cameroon itakayochezwa jijini Kampala kati ya
Machi 1 na 3 mwaka huu.
Orden
Mbaga ndiye atakayekuwa mwamuzi wa kati na atasaidiwa na mwamuzi
msaidizi namba moja Jesse Erasmo wakati mwamuzi msaidizi namba mbili ni
Hamis Chang’walu. Mwamuzi wa mezani ni Israel Mujuni na Kamishna wa
mechi hiyo atakuwa Souleiman Waberi wa Djibouti.
Wakati
huo huo, waamuzi kutoka Afrika Kusini ndiyo watakaochezesha mechi ya
kwanza ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa kati ya Simba ya Tanzania
na Clube Recreation Libolo ya Angola itakayofanyika Februari 17 mwaka
huu jijini Dar es Salaam.
Waamuzi
hao ni Daniel Volgraaff atakayepuliza filimbi wakati wasaidizi wake ni
Enock Molefe, Lindikhaya Bolo na Lwandile Mfiki. Kamishna wa mechi hiyo
atakuwa Emmanuel Lesita kutoka Lesotho.
No comments:
Post a Comment