KAMATI ya
Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imeiagiza Ofisi ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalumu wa
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), baada ya kuonekana kuna mtiririko wa
fedha usioeleweka kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda kwenye
bodi hiyo. Ofisi
ya CAG imetakiwa kufanya ukaguzi huo kwa hesabu za TTB kwa miaka mitano
iliyopita, kwani kuna Sh500 milioni zimekuwa hazina mtiririko
unaoeleweka kutoka wizarani kwenda TTB.
Kabla
ya kutolewa kwa agizo hilo, wajumbe wa kamati ya POAC wakiongozwa na
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola walihoji sababu za TTB kupata fedha
kutoka wizarani kwa ajili ya kushiriki maonyesho ya Sabasaba na
Nanenane, wakati mfumo wa serikali hauruhusu hilo.
Lugola
alimbana Mwenyekiti wa Bodi ya TTB, Balozi Charles Sanga akitaka atoe
ufafanuzi kuhusu fedha hizo zinazoingizwa kutoka wizarani kwenda TTB,
kwani inaonyesha huwa zinakwenda kinyume na utaratibu.
“Fedha
zinazofichwa TTB kutoka wizarani ni za nini, kwa nini Serikali
inahamisha fedha na kuingiza kwenu kinyume na utaratibu?” alihoji Lugola
na kuongeza: “Unajua kiasi cha Sh500 milioni ni nyingi sana.”
Aliendelea kutaka ufafanuzi zaidi akitaka TTB ieleze kama mfumo unaotumika unaruhusu TTB kupata fedha kutoka serikalini au la.
Akijibu
hoja hizo, Balozi Sanga alisema mfumo huo siyo sawa kwani mfumo wa
serikali na mashirika ya umma ni tofauti, hivyo kilichotokea ni makosa.
“Wizara
ndiyo inaweza kutusaidia ufafanuzi kuhusu hili, lakini nikuhakikishie
ni kwamba tunafanya kazi kwa karibu na wizara,” alisema Balozi Sanga.
Alisema hawezi kutoa jibu la wizara kupeleka fedha TTB, kwa sababu hana majibu. Akizungumzia
hilo, Mkurugenzi wa Utalii kutoka wizarani, Ibrahim Mussa alikiri kuna
fedha zimekuwa zikipelekwa TTB kwa ajili ya maonyesho hayo, ila kosa ni
kwamba sekretarieti ya maandalizi huwa iko wizarani, hivyo kusababisha
kuwa na kasoro za hapa na pale.
“Mwaka ujao tutazirekebisha kasoro hizo na kuhamishia shughuli zote TTB, kuna upungufu huo mwenyekiti nakiri,” alisema Mussa.
Mwenyekiti
wa POAC, Zitto Kabwe licha ya masuala hayo, alihoji kama TTB ina
mkataba na wizara wa kuwa wakala wao katika maandalizi ya Sabasaba na
Nanenane, wakati TTB ikijua ina uwezo wa kutangaza utalii yenyewe.
Mkurugenzi wa TTB, Dk Aloyce Nzuki alisema huwa wanapewa maelezo kutoka wizarani kufanya kazi hiyo.
No comments:
Post a Comment