Friday, January 18, 2013

WiLDAF; SERIKALI IMECHANGIA WANAFUNZI IFM KUDHALILISHWA

Kituo cha Sheria kwa Wanawake na Maendeleo ya Afrika (WiLDAF) kimesema kitendo cha wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kubakwa na kulawitiwa kinatokana na uzembe wa Serikali kutokuwa na bodi ya kusimamia ujenzi wa hosteli za wanafunzi ikiwa ni pamoja na kujenga ukuta mrefu na kuwa na walinzi wa kutosha.

Mkurugenzi wa kituo hicho, Dk. Judith Odunga, alisema jijini Dar es Salaam kuwa Serikali ilitakiwa kuweka bodi itakayosimamia ujenzi wa mabweni ya wasichana na wavulana tena kwa kiwango kinachotakiwa kisheria ikiwa ni pamoja na kujenga uzio mkubwa na kuweka walinzi wakutosha ili kuepuka madhara kama yaliyotokea kwa wanafunzi wa  chuo hicho kilichoko katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

“Jambo hili limeniuma sana na limetokana na uzembe wa serikali kutosimamia vema wamiliki wa hosteli kuwapa masharti ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi,” alisema.

Dk. Odunga alisema kuwa serikali inatakiwa kuwasimamia wamiliki wa hosteli ili vitendo vya wanafunzi kupigwa, kuibiwa, kulawitiwa na kubakwa kutojirudia tena katika hosteli zinazotumiwa na wanafunzi wa vyuo vikuu vingine.

Dk. Odunga pia alilaani kitendo cha baadhi ya askari polisi kutumia nguvu kubwa kuwatawanya wanafunzi kwa kuwapiga wakitumia viboko na mabomu na kusababisha baadhi yao kuzirai.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kitendo hicho kinakiuka haki za binadamu kwa kuwa binadamu ana haki ya kusikilizwa.

Jumatatu wiki hii, wanafunzi wa IFM walifanya maandamano makubwa jijini Dar es Salaam hadi katika ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakilalamikia Jeshi hilo kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya wizi, kulawitiwa na kubakwa, ambavyo wanafanyiwa na genge la wahuni katika hosteli yao iliyoko Kigamboni.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment