- Awalima watuhumiwa faini chapchap
- Atumia kibatari kuendesha kesi usiku
- Takukuru wamkamata
Hakimu wa
Mahakama ya Mwanzo Lupata katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Andrew
Siwale na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kisegese, Gasper Bagomoke,
wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa
tuhuma za kushirikiana kuanzisha mahakama bandia kinyemela. Hakimu
na Mtendaji huyo, wanadaiwa kuitumia mahakama hiyo kuendesha kesi
kuanzia jioni hadi usiku na kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa watu
ambao wanashtakiwa kwao.
Kwa
mujibu wa Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mbeya, Daniel Mtuka, watuhumiwa
hao walikamatwa juzi baada ya taasisi hiyo kufuatilia nyendo zao na
kubaini mambo wanayoyafanya kinyume cha sheria.
Alisema
kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja walishirikiana na kutumia jengo la Ofisa
Mtendaji wa Kata ya Kisegese kuanzisha mahakama bandia kinyemela ambayo
wamekuwa wakiitumia kusikiliza kesi kuanzia saa 12:00 jioni hadi 4:00
usiku.
Mtuka alisema Takukuru katika uchunguzi wake, ilifika kwenye ofisi za
Msajili wa Mahakama wa Wilaya ya Rungwe kujua uhalali wa mahakama hiyo
na kubaini kuwa haipo kwenye orodha za mahakama za mwanzo wilayani humo.
“Uchunguzi wetu umebaini kuwa mahakama hiyo iliyofunguliwa kinyemela,
huanza kazi zake za kusikiliza kesi kuanzia majira ya saa 12:00 jioni na
kuendelea hadi saa 4:00 usiku, kwa kuwa jengo la Ofisa Mtendaji ambalo
ndilo wanalitumia kufanyia shughuli zao halina umeme, watuhumiwa
walilazimika kuwasha vibatari ili wapate mwanga,” alisema Mtuka.
Kwa mujibu wa Mtuka, baada ya Takukuru kubaini uwepo wa mahakama hiyo,
maofisa wake waliweka mtego kwa kutumia mwananchi mmoja aliyekuwa na
kesi kwenye mahakama hiyo bandia ambaye alitakiwa kutoa rushwa ya Sh.
200,000 ili apewe upendeleo katika kesi iliyokuwa ikimkabili.
Alisema kuwa wakati watuhumiwa hao wakikabidhiwa fedha hizo na mwanachi
huyo, ambaye Mtuka hakutaka kumtaja jina kwa kuwa uchunguzi wa suala
hilo unaendelea, ndipo makachero wa Takukuru walipowakamata na
kuwapeleka katika ofisi za Takukuru wilayani Rungwe kwa mahojiano.
Kamanda Mtuka alisema kuwa Takukuru pia ilipata wananchi wengine zaidi
ya sita waliotoa ushahidi na malalamiko juu ya kudhulumiwa haki zao
kupitia mahakama hiyo bandia.
“Watuhumiwa wote tunawafikisha mahakamani leo (jana) mchana kwa sababu
taratibu zote za kuwafungulia kesi zimekamilika na tunao ushahidi wa
kutosha baada ya wananchi zaidi ya sita kujitokeza na kutupatia
ushirikiano wa kutosha kuhusiana na suala hili,” alisema Kamanda Mtuka.
Alisema tukio hilo limeishtua Takukuru Mkoa wa Mbeya na sasa imeamua
kuweka kipaumbele na kuelekeza nguvu zake katika mahakama za mwanzo na
kwenye mabaraza ya ardhi ya vijiji na kata ili kuibua uozo zaidi kwenye
maeneo hayo ambayo wanaamini kuwa wananchi wengi wanadhulumiwa haki zao.
Habari tulizozipata baadaye jana zinaeleza kuwa watuhumiwa hao
walisomewa mashitaka katika Mahakama ya Wilaya ya Rungwe, na kwamba
walikana na kuachiwa kwa dhamana hadi Februari 13, mwaka huu kesi hiyo
itakapotajwa tena.
No comments:
Post a Comment