KAMATI ya
Hesabu za Mashirika ya Umma (Poac), imelitaka Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania (TPDC), kuwasilisha kwenye kamati hiyo mikataba
iliyoingiwa na Serikali kuhusu ujenzi wa bomba la gesi la Mtwara hadi
Dar es Salaam ili ipitiwe upya. Mbali
na uamuzi huo, kamati hiyo imeitaka Serikali itoe elimu kwa wakazi wa
mikoa ya kusini kuhusu mradi huo ili kuondoa mgogoro uliokwishajitokeza.
Kamati
hiyo ilitoa maagizo hayo jana baada ya wajumbe wake kubaini kuwa kuna
makubaliano yasiyo rasmi baina ya Serikali na makandarasi wa bomba hilo,
jambo ambalo linaweza kuitia hasara Serikali.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Zitto Kabwe alisema TPDC inapaswa kuwasilisha mikataba
hiyo kabla ya kumalizika kwa kikao kijacho cha Bunge ili waweze kuipitia
upya na kujiridhisha.
“Tumewaambia
TPDC watuletee mkataba wa ujenzi wa bomba la gesi la Mtwara. Hii
itasaidia kuangalia makubaliano yaliyoingiwa kati ya Serikali na
mkandarasi, jambo ambalo linaweza kutusaidia kubaini kama una utata au
la,” alisema Zitto.
Alisema
hatua ya kupitia upya mikataba hiyo itasaidia kubaini upungufu uliopo
na kuufanyia kazi, kabla ya kuanza mradi huo ili kuokoa fedha ambazo
zingeweza kupotea kutokana na tatizo la ubovu wa mikataba.
“Lengo
la kufikia uamuzi huo ni kuangalia mkataba huo kama umefuata hatua za
kisheria au la, maana mkataba uko wizarani na TPDC hawana nakala, wakati
ndiyo wanaosimamia mradi huo, sasa kuna usiri gani hapo?” alihoji
Zitto.
Mjumbe
wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza
Mangungu alisema kitendo cha TPDC kutokuwa na mkataba huo wakidai uko
wizarani, kinaonyesha kuwa kuna jambo lisilo la kawaida.
Akizungumzia
sakata la wananchi wa Mtwara kuandamana, Mangungu alisema kitendo kile
kinatokana na Serikali kushindwa kuwaelimisha wananchi wa maeneo
yanayopitiwa na mradi huo.
“Serikali
ilipaswa kuwaelimisha wananchi wa Mtwara kuhusu gesi, hii ingesaidia
kuamini kuwa mradi huo bado haujakamilika na wanapaswa kusubiri lakini
wamekaa kimya, badala yake wananchi wanaamini kuwa umekamilika na kwamba
hawawezi kunufaika na kitu chochote, jambo ambalo limesababisha
waandamane,” alisema.
Mkurugenzi wa TPDC, Yona Kilagane alisema mkataba baina ya kampuni inayojenga bomba hilo na Serikali uko wizarani.
“Sisi
hatuna mkataba wa ujenzi wa bomba hilo mkataba wake uko wizarani, kazi
yetu ni kusimamia na kushirikiana na kampuni inayoendesha mradi kwa
ajili ya ujenzi wa bomba hilo,” alisema Kilagane.
Mwaka jana, Serikali ilizindua ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilometa 532 ambao utakamilika kabla ya mwaka 2014.
Kampuni
zilizoiingia mkataba wa ujenzi wa bomba hilo ni Shirika la Maendeleo ya
Teknolojia ya Petroli China, Shirika la Uhandisi wa Bomba la Petroli na
Shirika la Uhandisi wa Bomba la Petroli la China.
Mradi huo utagharimu kiasi cha Dola 1.86trilioni ambazo ni fedha za mkopo kutoka Benki ya Exim ya China.
Mpango huo utahusisha ujenzi wa bomba la inchi 36 kwa umbali wa kilometa 487 na bomba la nchi 24 la umbali wa kilometa 24.
Historia ya sakata la gesi
Desemba 27 mwaka jana, mamia ya wakazi
wa Mkoa wa Mtwara waliandamana wakipinga uamuzi wa Serikali kusafirisha
gesi kwa njia bomba kwenda Dar es Salaam.
Maandamano hayo yalianzia katika
Kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara mjini kupitia barabara ya Msimbati, eneo
ambako gesi asilia inapatikana.
Waandamanaji hao waliotembea umbali wa
kilometa tisa, walitoa maazimio tisa huku mojawapo likihoji sababu za
mitambo ya kuzalisha umeme kutojengwa Mtwara ambako ni jirani na
inakochimbwa gesi asilia.
Waandamanaji hao walitaka mradi wa kuzalisha umeme wa gesi asilia kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam usitishwe.
Walitaka vinu vya kuzalishia umeme wa
gesi vijengwe Mtwara kwa kuwa wanayo maeneo ya kutosha ya ujenzi huo
tofauti na Dar es Salaam.
Walisema
wanahitaji viwanda vikubwa vijengwe Mtwara ili kuleta ajira kwa wakazi
wa Mtwara na mikoa ya jirani na kwamba wana hofu ya kubaki maskini kama
wakazi wa Songosongo mkoani Lindi ambako walisema licha ya kuvuna gesi
wamebakia na umaskini.
Maandamano
hayo yaliratibiwa na vyama vya siasa vya Chadema, NCCR-Mageuzi, Sau,
TLP, APPT Maendeleo, ADC, UDP na DP yakiwa na kaulimbiu ya ‘gesi kwanza
vyama baadaye, hapa hakitoki kitu.’
Waandamanaji
hao waliungwa mkono na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa CCM Mkoa
wa Mtwara ambao walipinga usafirishaji wa gesi kwenda Dar es Salaam.
Hata
hivyo, akihutubia taifa katika salamu za mwaka, Rais Jakaya Kikwete
alisema Serikali haitasitisha mpango wake wa kusafirisha gesi kutoka
Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Alisema
Serikali itaendelea na mpango huo kwa sababu rasilimali yoyote
inapogundulika sehemu yoyote katika Tanzania inakuwa mali ya Watanzania
wote.
Alisema
suala la kusitisha usafirishaji wa gesi halikubaliki lakini akaahidi
kuwa wananchi wa Mtwara watanufaika na mradi huo kama walivyo wengine.
Mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alilazimika kukatisha ziara mkoani Mtwara
baada ya kushushwa jukwaani alipotoa kauli zilizowakasirisha wakazi
huko kuhusu gesi.
Mbatia
alishushwa jukwaani na wafuasi wa NCCR kabla hajamaliza kuhutubia ili
kumhami na baadhi ya vijana walioanza kumrushia mawe wakidai
kutoridhishwa na hotuba yake iliyokuwa na mwelekeo tofauti nao wao
kuhusu usafirishwaji wa gesi hiyo.
No comments:
Post a Comment