Mawaziri
kutokana na wabunge limezidi kuwa la moto, baada ya Jaji Mkuu mstaafu,
Barnabas Samatta, na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kuungana na
Spika wa Bunge, Anne Makinda, kupendekeza Katiba Mpya ijayo izuie mfumo
huo. Jaji
Samatta na Sumaye, walipendekeza hivyo kwa nyakati tofauti, ikiwa ni
sehemu ya maoni yao waliyoyatoa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, jijini
Dar es Salaam, juu ya uundwaji wa Katiba Mpya.
Mbali
na hayo, Jaji Samatta pia alipendekeza Katiba Mpya itamke namna ya
kupata chombo kitakachofanya kazi ya kuwafundisha wananchi katiba ya
nchi.
Pia alipendekeza utaratibu wa kupata viongozi mbalimbali wa serikali
ubadilike ingawa hakusema namna utakavyokuwa ndani ya Katiba Mpya.
Vilevile, alipendekeza utaratibu wa kuwapata majaji ubadilike ili kutoa
manung’uniko yanayotolewa na wananchi juu ya uteuzi wa watumishi hao wa
umma.
Kuhusu Muungano, Jaji Samatta alikataa kueleza maoni yake, badala yake alisema suala hilo ni la kisiasa zaidi.
MAONI YA SUMAYE
Sumaye alisema japo watu wengine wanadhani mawaziri kutokuwa wabunge
itakuwa na gharama, lakini akasema itasaidia serikali na Bunge kufanya
kazi na kuwaondoa wale wanaotegemea uwaziri kupitia ubunge.
Pia alipendekeza Katiba Mpya itamke wakuu wa mikoa na wilaya wasiwe
wanasiasa kama ilivyo sasa, badala yake wawe watumishi wa umma.
Alisema kwa kuwa siasa inakuwa na kwamba, katika siku za usoni lazima
mfumo utabadilika na kuongozwa na vyama vingine vinavyoweza kuwatoa wote
madarakani kwa kuwa ni wanasiasa, ni vyema eneo hilo liwe la kiutumishi
badala ya siasa.
Vilevile, alisema hakuna anayetaka madaraka ya rais yapunguzwe, badala yake yaboreshwe ili kumfanya anga’are na atakate.
“Siyo kila watu ateue. Na ninachosema hapa si kumpunguzia nguvu. Ila
nafasi za gavana, mwanasheria mkuu, katibu mkuu kiongozi na jaji mkuu
nafasi zao zipite kwenye ngazi fulani kisha uteuzi wao uthibitishwe na
Bunge,” alisema Sumaye.
Kuhusu Muungano, Sumaye alisema ni suala gumu na kama ingewezekana
kungekuwa na sura ya serikali moja, lakini kwa sasa ni gumu, hivyo
akataka ubaki kama ulivyo.
Hata hivyo, alipendekeza uboreshwe, hasa katika maeneo yenye manung’uniko.
Kwa upande wa serikali tatu, alisema Muungano huo hautadumu kwa sababu
uchumi wote utakuwa kwa Serikali ya Muungano na si serikali ya mapinduzi
Zanzibar na ya Tanganyika.
“Ikiwa serikali tatu hali itakuwa tete sana maana Muungano atamiliki
rasilimali watu na uchumi na hawa wengine kubaki wakiwa hawana vyote na
matatizo yakianza muungano utavunjika, Serikali moja ni nzuri sana
lakini hatuwezi kurudi nyuma”alisema.
MAONI YA MALECELA
Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela, alipendekeza Katiba Mpya itambue
mabunge mawili, badala ya moja na kuacha kugusa madaraka aliyonayo rais.
Alitoa kauli hiyo jana alipofika katika ofisi za Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kutoa maoni yake.
Alisema kuwapo mabunge mawili ni muhimu, hususani kwa nchi zinazoendelea
na kwamba, yanasaidia kuchambua baadhi ya mambo kwa undani.
Malecela alisema ametoa maoni kwamba, madaraka ya rais yaachwe kama
yalivyo kwa kuwa ni muhimili unaojitegemea. Alihoji kwamba, ikiwa
madaraka hayo yatapunguzwa yatapelekwa katika muhimili upi?
“Hapa tunapunguza madaraka ya rais halafu tunayapeleka wapi kwa kuwa
mihimili mingine ya Mahakama na Bunge inajitegemea na haiwezi kupelekewa
madaraka hayo?” alihoji Malecela.
Alisema kwa nchi changa kama Tanzania, bado kuna haja ya rais kuwa na
madaraka makubwa ili kumuwezesha kuisimamia nchi anayoiongoza.
Alipendekeza Katiba Mpya itambue nafasi za viti maalum za ubunge kwa wanawake ili kufikia idadi ya asilimia 50 kwa 50.
Alisema kinacholalamikiwa katika nafasi hizo, ni namna zinavyopatikana, lakini siyo umuhimu wake kwa maendeleo ya taifa.
Wakati Malecela na Sumaye wakitaka madaraka ya rais yasipunguzwe, mapema
wiki hii Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, naye alitoa
mapendekezo kama hayo na kusema kwamba, unahitajika umakini katika
kutekeleza suala hilo.
Balozi Sefue alisema iwapo maamuzi yoyote juu ya suala hilo
yatachukuliwa kiholela, kuna hatari rais akashindwa kuwashika Watanzania
pamoja kama taifa.
Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam
wiki hii, muda mfupi baada ya kuongoza makatibu wakuu wa wizara, katika
mkutano na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwa ajili ya kutoa maoni juu ya
uundwaji wa Katiba Mpya.
Balozi Sefue alisema madaraka ya rais wa nchi kama Tanzania yenye mifumo
changa, hayapaswi kudhoofika kwa namna yoyote, badala yake yanatakiwa
kuwa imara kwa kuwa ndiye anayehodhi mamlaka ya nchi.
“Hivyo, tusije kumpunguzia madaraka rais kiasi, ambacho akashindwa
kutushika pamoja kama taifa. Tusiwe wepesi kusema punguza, punguza
madaraka ya rais,” alisema Balozi.
Kabla ya Balozi Sefue na Malecela kusema hayo, tayari baadhi ya makundi
katika jamii, wakiwamo wanasiasa, wanaharakati, wafugaji nakadhalika,
wamekuwa wakipendekeza kuwapo na udhibiti mkubwa wa mamlaka ya rais.
Katika mapendekezo yao, makundi hayo yanataka pamoja na mambo mengine,
rais asiwe na mamlaka ya kuteua viongozi wa mihimili mingine ya dola
peke yake na asiruhusiwe kusamehe wafungwa na watuhumiwa.
Pia kila atakayeteuliwa na rais lazima aombe kazi husika kwenye tume
huru za kitaalamu na athibitishwe na Bunge, pia rais asiteue Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) na asiwe na mamlaka ya ardhi.
JAJI WARIOBA: MAKUNDI 80 YAMESHATOA MAONI
Akizungumzia mchakato wa utoaji wa maoni, Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alisema hadi sasa makundi
maalum 80 yameshatoa maoni.
Alisema kwa siku wastani wa makundi tisa yalikuwa yanatoa maoni yao na
kwamba, ifikapo mwisho wa mwezi huu makundi yote yatakuwa yamemaliza
kutoa maoni.
Jaji Warioba alisema mwezi ujao Tume itaanza kuchambua maoni yote
yaliyotolewa na wananchi na kwamba, baada ya hapo wataandika rasimu ya
Katiba Mpya.
Alisema rasimu inatarajiwa kukamilika Juni, mwaka huu, ambayo itapelekwa
kwenye mabaraza ya katiba kwa ajili ya kupitiwa. Aliwahakikishia
Watanzania kwamba, malengo ya kupatikana Katiba Mpya kabla ya Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2015, yatafikiwa kwa kuwa wako ndani ya muda waliopangiwa.
No comments:
Post a Comment