Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeshindwa kueleza kama imetekeleza
agizo la Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuhakikisha
inaiondoa meli ya Mt. Al Biraq katika ardhi ya Tanzania ndani ya saa
24. Meli
hiyo yenye namba za usajili IMO 9381732 iliamriwa kuondoka nchini juzi
kutokana na kuingiza mafuta ya dizeli ambayo hayana viwango vya ubora. Mfuta
hayo ambayo ni tani 100,010 yalibainika kuwa hayafai baada ya Shirika
la Taifa la Viwango Tanzania (TBS) kuyapima na kubaini hayana viwango
vya ubora.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande, akizungumza na NIPASHE jana
kama agizo la Waziri limetekelezwa, alisema kiutaratibu meli inakuwa
chini ya uangalizi wa TPA pale inapokuwa ndani ya bandari.
Kipande hata hivyo, hakuweza kufafanua kama anamaanisha kuwa meli hiyo
haikuwa ndani ya bandari, alisema agizo la waziri atakaporudi ofisini
kwake ataliangalia.
“Kwa kuwa nipo nje ya ofisi, nikirudi ofisini nitaliangalia na kukupigia simu kukujulisha,” alisema Kipande.
Hata hivyo, baadaye NIPASHE ilipomtafuta Kipande kwa kumpigiwa simu,
alijibu kwa kifupi kuwa hana muda wa kuelezea suala la meli na kukata
simu.
Awali Kipande alisema kurejea kwa meli hiyo ikiwa na shehena ya mafuta
yaliyokataliwa mwaka jana kulisababisha mvutano baina ya baadhi ya
taasisi.
Juzi Dk. Mwakyembe alisema meli hiyo iliwasili nchini Desemba 27, mwaka
jana ikiwa na shehena ya tani 100,010 ya dizeli, lakini ikagundulika
kuwa mafuta hayo hayana ubora na kutakiwa kurejea nayo yalikotoka.
Siku tisa baadaye yaani Januari 5, mwaka huu ilirejea nchini ikiwa na
shehena ile ile kwa nia ya kudanganya mamlaka za Tanzania ili kuruhusiwa
kuuza mafuta katika soko la Tanzania.
Alisema kuwa Januari 15, mwaka huu meli hiyo baada ya kuingiza mafuta
hayo yalipimwa na TBS na kukuta matatizo yale yale na hivyo kuagiza
yasiingizwe nchini kutokana na kuwa chini ya viwango vya ubora.
No comments:
Post a Comment