Aliyekuwa
waziri matata wa vijana na mshirika mkubwa wa aliyekuwa rais Laurent
Gbagbo, Charles Ble Goude, amekamatwa nchini Ghana. Bwana
Ble Goude anakanusha madai ya kuongoza wapiganaji waliowashambulia raia
wa kigeni na raia kutoka Kaskazini mwa nchi wakati wa uchaguzi
uliokumbwa na utata mwaka 2010. Amekuwa mafichoni tangu Aprili mwaka 2011, wakati Gbagbo alipokamatwa.
Gbagbo anasubiri kusikilizwa kwa kesi yake katika
mahakama ya kimataifa ya jinai huko Hague akikabiliwa na makosa ya
uhalifu dhidi ya binadamu.
Watu elfu
tatu walipoteza maisha yao katika mzozo huo uliodumu miezi minne wakati
Gbagbo alikataa kuondoka mamlakani baada ya kushindwa.
Washirika kadhaa wa Gbagbo wamekimbilia uhamishoni nchini Ghana na mwanzo waliripoti kuwa bwana Ble Goude amekamatwa.
"naweza
kuthibitisha kuwa tumemkamata mtu tunaye amini kuwa waziri wa zamani wa
vijana nchini Ivory Coast.'' alisema Larry Gbevlo-Lartey, katibu wa
usalama.
"kuna
waranti ya kumkamata na tumekuwa tukimsaka kwa muda mrefu sana. Tungali
tunatafuta habari zaidi na kisha tutaweza kumkabidhi kwa serikali,''
aliongeza katibu huyo.
Mwaka jana
aliambia BBC kuwa kama kiongozi wa vijana yeye aliandaa tu mikutano ya
hadhara na wala hakuwahi kuwa kiongoizi wa wapiganaji.
"mimi sio
kiongozi wa wapiganaji, sijawahi kununua silaha tullifanya maandamano
dhidi ya wale waliokuwa na silaha, hatukuwa tumebeba chochote,'' alisema
Ble Goude
Alisema kuwa yuko tayari kwenda katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita kujiondolea lawama.
Bwana Ble
Goude aliwekewa vikwazo na Umoja wa mataifa mwaka 2006 akituhumiwa kwa
kuchochea mashambulizi dhidi ya maafisa wa umoja huo.
Chanzo - BBC Swahili
No comments:
Post a Comment