HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete na Rais
Paul Kagame wa Rwanda, jana walikutana ana kwa ana mjini Kampala nchini
Uganda. Hii ni mara ya kwanza viongozi hao kukutana, baada ya kuwapo na
uelewano mdogo kutokana na Rais Kikwete kumshauri Rais Kagame akutane na
vikundi vya waasi vinavyopigana mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Baada ya kutolewa ushauri huo, Rais
Kagame alionekana wazi kutoukubali, jambo ambalo limezua mambo mengi
yakiwamo ya wafanyabiashara wa nchi yake kutangaza kutotumia Bandari ya
Dar es Salaam kupitishia mizigo yao.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya
habari na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu mjini Dar es Salaam jana,
ilisema viongozi hao walikutana faragha katika mazungumzo yaliyokwenda
vizuri.
“Viongozi wamekutana kwa saa moja katika
mkutano uliofanyika kwenye Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort, nje
kidogo ya mji wa Kampala.
“Katika mazungumzo hayo, wamekubaliana
kuendelea kushirikiana kujenga uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo
kati ya nchi hizo mbili,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo, ilisema viongozi wako
nchini Uganda kuhudhuria Mkutano wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Kimataifa
wa Maziwa Makuu, ulioanza jana katika Hoteli ya Munyonyo Commonwealth
Resort.
Viongozi wengine ambao wanahudhuria
mkutano huo, ni pamoja na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye ni
Mwenyekiti wa ICGLR, Rais wa Sudan Kusini, Silva Kiir, Rais wa Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila na Mwenyekiti wa Kamisheni
ya Umoja wa Afrika (AU).
Uhusiano huo, ulizidi kuingia doa baada
ya Serikali ya Rwanda kuamua kupandisha ushuru mpya kutoka dola 152 za
Marekani hadi dola 500 kwa malori ya Tanzania pekee.
Katika hali ya kushangaza, Serikali ya
Rwanda ilisema ushuru huo utatumika kwa kipindi cha wiki moja, jambo
ambalo halikukubalika.
Lakini Msemaji wa Umoja wa Wasafirishaji
Malori Tanzania (TATOA), Elias Lukumay alisema kuna hatari kubwa ya
kupoteza wateja wao kutokana na tozo mpya.
Alisema kama tozo hiyo ikiendelea
kutozwa, wafanyabiashara wa malori Tanzania wataathirika kwa kuwa
watalazimika kupandisha bei ya usafirishaji karibu dola 500.
No comments:
Post a Comment