IMEVUJA! Staa muuza nyago kwenye video
za wasanii wa muziki wa kizazi kipya na filamu za Kibongo, Agnes Gerald
‘Masogange’ na shosti wake, Mellisa Edward kabla ya kupandishwa
kizimbani kwa msala wa dawa za kulevya ‘unga’ Afrika Kusini waliingizwa
kwenye chumba cha mateso kwa saa 24 ili kutaja waliowatuma.
Habari kutoka kwa chanzo chetu kilichopo
jijini Johannesburg nchini humo zilidai kuwa baada ya kukamatwa katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, walipelekwa polisi ambapo
walichukuliwa maelezo.
Ilielezwa kuwa mwanzoni waligoma kueleza
mzigo huo wa kilo 150 wa unga ulikuwa wa nani hivyo ikabidi polisi wa
upelelezi watafute njia nyingine ya kuwalainisha kwa kuwabembeleza kuwa
wakieleza ukweli wataachiwa.
MATESO SAA 24
Chanzo hicho kilisema kuwa baada ya
mbinu hiyo kushindikana ndipo wawili hao wakaingizwa kwenye chumba
maalum cha mateso ikiaminika kuwa watasema aliyewatuma.
USHUHUDA
“Unajua Sauzi (Afrika Kusini) huwa
hawana utani na ishu za madawa ya kulevya. Jamaa (polisi) wana kila aina
ya mbinu ya kumfanya mtu aeleze ukweli.
“Katika kutesa unaweza kuingizwa kwenye chumba maalum cha mateso ambayo nayo huwa yana steji zake.
“Kwanza utaanzia kwenye chumba
kilichojazwa siafu wakubwa na huko unaweza usijue kuwa kuna siafu zaidi
ya kuona kitu kama red carpet (zuria jekundu) kuanzia sakafuni, ukutani
hadi kwenye dari, kumbe wale wote ni siafu.
“Wakishakuingiza mle ndipo utashangaa
wale siafu wanacharuka na kuanza kukung’ata mwili mzima, zoezi hilo
hufanyika kwa saa 24. Lazima useme ukweli.
“Kama bado ukijifanya mbishi au nunda
ndipo unapelekwa hatua nyingine ya kulazimishwa kujisaidia haja ndogo
kwenye waya wa umeme.
“Si unajua tena waya wenye umeme na maji
vikikutana nini kinatokea? Lazima itatokea shoti ya kutisha kwani ule
waya hufuata sehemu yale maji yanapotokea.
“Kinachofuata ni mtu kupigwa shoti kali ya umeme ambapo lazima utasema tu.
“Hicho ndicho kilichowapata akina Masogange kama wanavyofanyiwa Wabongo wengine wanaokamatwa Mitaa ya Rissik hapa Johannesburg.
WALIOWATUMA
“Baada ya mateso hayo, waliwataja
waliowatuma mzigo huo wa unga aina ya crystal methamphetamine wenye
thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 6.8,” kilisema chanzo hicho ambacho ni
Mbongo ambaye kwa sasa ni mkazi wa Mtaa wa Rissik, Johannesburg,
wanapoishi Wabongo kwa kuungaunga aliyewahi kukumbwa na mkasa kama huo.
MTOTO WA KIGOGO ATAJWA
Habari za ndani zilidai kuwa baada ya
kupitia mateso hayo, mabinti hao waliwataja watu wawili waliowatuma
kusafirisha mzigo huo, mmoja akiwa ni mtoto wa kigogo ambaye ni
mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania (jina lipo).
Ilidaiwa kuwa mtoto huyo wa mkubwa ni
mjanja wa mjini ambaye alihusika kushughulikia kusafirisha mwili wa
msanii Albert Mangweha ‘Ngwea’ aliyefia Johannesburg Juni, mwaka huu.
Ilivuja kuwa mwingine aliyetajwa na
akina Masogange ni mfanyabiashara maarufu Bongo anayesafiri nje mara kwa
mara huku jina la ‘mtoto wa mjini’ Mangunga likitajwa zaidi hata na
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison George Mwakyembe.
Gazeti hili lilipozungumza na Kamanda wa
Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya, Godfrey Nzowa,
alikiri kupewa majina hayo lakini akaliomba gazeti hili kutoyachapisha
kwa sasa kuepuka kuvuruga ushahidi.
ULINZI KAMA SHEHE PONDA
Baada ya polisi wa upelelezi na wale wa
kimataifa (Interpol) kujiridhisha na maelezo ya mabinti hao,
walipandishwa kizimbani kwa mara ya pili Agosti 19, mwaka huu chini ya
ulinzi mkali kama ule ‘anaowekewaga’ Katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Tanzania, Shehe Ponda Issa Ponda anapofikishwa kwenye mahakama
mbalimbali nchini kwa kesi zake za madai ya uchochezi.
WAPANDISHWA TENA KORTINI
Habari kutoka Sauzi zilieleza kuwa akina
Masogange walipandishwa tena kizimbani hivi karibuni ambapo tayari kesi
yao imeanza kuunguruma ikielezwa kuwa endapo watakutwa na hatia
watakula mvua ya kifungo si chini ya miaka 10 kwa sheria za nchi hiyo.
Masogange na Mellisa walinaswa nchini humo Julai 5, mwaka huu wakiwa na mabegi sita yaliyokuwa na mzigo huo wa unga.
No comments:
Post a Comment